Home » » Deo Mwanambilimbi, Wenzake Wawili Mbaroni kwa Uhamiaji Haramu

Deo Mwanambilimbi, Wenzake Wawili Mbaroni kwa Uhamiaji Haramu

Written By Bewith Jeddy on Sunday, February 14, 2016 | 9:32 AM

Deogratius ‘Deo’ Mwanambilimbi
IDARA ya Uhamiaji imewatia mbaroni wanamuziki mashuhuri Deogratius ‘Deo’ Mwanambilimbi, rapa maarufu Alain Mulumba Kashama na Mwenabantu Kibyabya Michel wakihusishwa na uhamiaji haramu katika kutekeleza kauli mbiu ya Rais John Magufuli ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Mbali ya kuwakamata wanamuziki hao, Uhamiaji pia imemtia mbaroni Abdulahi Suleiman Mberwa kwa kosa la kujihusisha na biashara haramu ya kusafirisha binadamu kuwapeleka nje ya Tanzania.
Naibu Kamishna wa Uhamiaji nchini, John Mfumule, amewaambia waandishi wa habari leo kwamba, Mwanambilimbi anakabiliwa na kosa la kuajiri na kuwafanyisha kazi wageni – Alain Mulumba (39) na Mwenabantu Michel (35) wote raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo – katika bendi yake ya Kalunde huku akijua wanamuziki hao hawana vibali vya kazi na ukaazi.
Mwanambilimbi (43), mkazi wa Goba-Kinondoni jijini Dar es Salaam, ndiye mmiliki wa bendi ya Kalunde ambayo ina mkataba wa kutumbuiza kwenye hoteli ya Giraffe ya jijini humo.
“Kashama na Michel wote kwa pamoja wanakabiliwa na kosa la kuishi nchini na kufanya kazi bila kuwa na vibali,” alisema Naibu Kamishna Mfumule.
Inaelezwa kwamba, Kashama anamiliki hati ya kusafiria ya DR Congo yenye Namba OBO782268 iliyotolewa Aprili 21, 2015 itakayomalizika muda wake Aprili 20, 2020. Hati yake ya zamani ya kusafiria ni Namba C0172419 iliyotolewa Juni 12, 2008 na ilimalizika muda wake Juni 11, 2011.
Mwenabantu Michel ana hati Namba OBO487018 iliyotolewa Machi 29, 2008.
Hata hivyo, Kashamba ni miongoni mwa wanamuziki wakongwe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aliyeingia nchini Tanzania mwishoni mwa miaka ya 1990 na mwanzilishi wa bendi ya Diamond Sound ‘Wana Dar es Salaam Ikibinda Nkoi’ iliyokuwa ikilimikiwa na mfanyabiashara Fred Rwegasira ikiwa na makao yake makuu Silent Inn, Mwenge, ingawa kwa sasa haipo kwenye ulimwengu wa muziki.
Baada ya kusambaratika, wanamuziki wa bendi hiyo wakaanzisha bendi nyingine iliyojulikana kama Diamond Musica International.
Ni miongoni mwa wanamuziki walioleta mabadiliko ya muziki nchini kwa kuingiza rap, ghani ambazo zimeteka bendi nyingi za muziki wa dansi kwa sasa na kuvutia mashabiki wengi.
Baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakiunda bendi hiyo kabla ya kusambaratika ni Hassan Liver, Richard Mangustino, Wayne Zola Ndonga na aliyekuwa kiongozi wa bendi hiyo, Ibonga Katumbi ‘Jesus’.
Kwa upande mwingine, Abdulahi Mberwa (37), mkazi wa Kisauni, Zanzibar ambaye kwa sasa anaishi Magomeni Mapipa jijini Dar es Salaam, yeye anakabiliwa na makosa ya kuwasafirisha wasichana wa Kitanzania kwenda Arabuni, kosa ambalo ni la usafirishaji haramu wa binadamu.
Lakini pia anakabiliwa na kosa la kutoa nyaraka za uongo za wasichana ili kuwapatia hati za kusafiria na kuwapeleka huko Arabuni.
Mberwa alikamatwa pamoja na wasichana wawili ambao alitaka kuwasafirisha ambao ni Asma Halfe Mkeyenge (26), mkazi wa Tandika Davis Corner jijini Dar es Salaam na Nyamizi Halfa Kambunga (31), mzaliwa wa Urambo mkoani Tabora na mkazi wa Mbagala Misheni (KTM) jijini Dar es Salaam.
Naibu Kamishna Mfumule alisema kwamba, Asma aliwasilisha nyaraka za uongo ili kujipatia hati ya kusafiria yenye namba AB 402133 iliyotolewa Februari 9, 2026 ambayo inakwisha muda wake Februari 8, 2016, wakati Nyamizi naye aliwasilisha nyaraka za uongo na kujipatia hati ya kusafiria namba AB 402592 iliyotolewa Februari 10, 2016 na matumizi yake yanakwisha Februari 9, 2026.
Watu hao wote sita tayari wamekwishafikishwa mahakamani.


0 comments :

Post a Comment