Home » » Zitto Kabwe aibua Kashfa Nzito ya Ufisadi wa trioni 1.2 Serikali ya JK

Zitto Kabwe aibua Kashfa Nzito ya Ufisadi wa trioni 1.2 Serikali ya JK

Written By Bewith Jeddy on Tuesday, December 1, 2015 | 1:00 PMKiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo

SERIKALI ya Uingereza kupitia shirika lake la kuchunguza makosa ya jinai (AFO), imeibua kashfa ya rushwa katika ununuzi wa dhamana (hati fungani) ya serikali katika kipindi cha uongozi wa aliyekuwa Rais Jakaya Kikwete.
Madai hayo yametolewa jijini Dar es Salaam jana na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, katika taarifa yake aliyoisambaza kwenye vyombo vya habari jana.
Katika taarifa yake hiyo, Zitto alidai kuwa biashara hiyo iliyofanyika kati mwaka 2011 na 2012, iliyohusisha serikali na benki ya Standard Group ya Afrika Kusini kupitia Stanbic ya Tanzania ilikuwa na thamani ya Dola za Marekani milioni 600 (sawa Sh. Tanzania trioni 1.2).
Benki ya Standard Group ambayo ni benki mama ya Stanbic Tanzania, imekiri makosa hayo na kukubali kulipa faini ya Dola milioni 25.2 (sawa na Sh. bilioni 54 ) kwa kosa hilo.
Ilikubali kulipa faini hiyo mbele ya Jaji Lord Justice Leveson, wakati shauri hilo liliposikilizwa jana kwenye Mahakama ya Southwark nchini Uingereza.
Benki hiyo ilikubali shauri hilo limalizwe kwa njia ya muafaka baada ya kukiri ilitoa kiasi cha fedha ili kuwahonga maofisa wa Tanzania kinyume na Sheria ya Rushwa ya Uingereza ya mwaka 2010 kufanikisha mpango wao.
Pia benki hiyo imekubali kulipa kiasi cha Dola milioni saba (sawa na Sh. bilioni 15.1) kwa Serikali ya Tanzania kama fidia ya shauri hilo baada ya kubainika walihonga baadhi ya maofisa wa Tanzania kufanikisha mpango huo.
Hata hivyo, fedha hizo hazitakabidhiwa moja kwa moja kwa Serikali ya Tanzania bali zitapitishwa kwenye Wizara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza ili kupangiwa kazi ya kufanya.
Pia benki hiyo inatakiwa kulipa kiasi cha pauni 300,000(sawa na Sh. milioni 974) ikiwa ni gharama za shauri hilo kusikilizwa nje ya mahakama.
Katika taarifa yake, Zitto alitaka mamlaka zenye kuchunguza sakata hilo ikiwamo Benki Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Kudhibiti Biashara Haramu ya Fedha (FIU) Tanzania na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (Takukuru) waungane na SFO kutoa  taarifa za chunguzi huo na sababu ya kutoziweka hadharani mapema.
Aliomba vyombo vya sheria kuwachukulia hatua wote waliohusika na upotevu fedha hizo za Watanzania.
Alisema hati fungani hiyo ya serikali iliuzwa na serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa benki hiyo ya kigeni ambayo ni miongoni mwa kundi la mabenki ya Afrika ya Kusini, yenye makao makuu yake London, Uingereza.
Alisema ni jambo la kawaida duniani serikali kuuza dhamana zake za hati fungani, lakini kwa Tanzania uligubikwa na harufu ya rushwa na kuisababishia nchi hasara.
Alidai kuwa kwa mujibu wa uchunguzi huo, sehemu ya fedha hizo hazikuingia kwenye akaunti za Serikali ya Tanzania na pia gharama za hati fungani hiyo zilipaishwa kupitia wakala wa kati.
Kutokana na upaishaji wa gharama hizo, takriban Dola milioni 60 zilitolewa kwa maofisa waliothibitisha biashara hiyo.
Zitto alimuomba Rais Dk. John Magufuli, kuingilia kati suala hilo akisema jambo hilo lina maslahi mapana ya nchi, hasa ikizingatiwa na uzoefu katika masakata kama hayo yanayohusisha nchi za kigeni, kama ununuzi wa rada, vyombo vya uchunguzi vya hapa nchini, vilitoa majibu ya kutokuwapo kwa rushwa na kisha kuja kuthibitishwa na Serikali ya Uingereza.
“Baada ya kuthibitishwa na Uingereza, serikali yetu ilirudishiwa sehemu ya fedha zilizozidi kwenye manunuzi ya rada, ni vyema Rais Magufuli akaliingilia kati,” alisema Zitto.
Alisema ACT-Wazalendo inasubiri taarifa ya makubaliano kati ya SFO na benki mama ya iliyonunua hati fungani hiyo ili ashauri zaidi hatua za kuchukua.
“Ikumbukwe kuwa Benki ya…(anaitaja jina), ilihusika na kashfa ya Tegeta Escrow na mpaka sasa haijachukuliwa hatua zozote kama ilivyoagizwa na Bunge. Benki hiyo imewaficha waliochota fedha za Escrow mpaka leo,” alisema Zitto.
Alisema kashfa hiyo iliwafanya washauri uongozi wa benki hiyo hapa nchini kuondolewa na kurejeshwa nchini Uingereza kwa hatua zaidi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Hazina, Ramadhani Kijja, alisemakuwa halifahamu suala hilo na kwamba kwa sasa hana maelezo yoyote juu ya jambo hilo.
“Kama Zitto ndiye katoa hiyo taarifa, mimi sina na wala siwezi kuizungumzia kwa sasa,” alisema Kijja.

Source: GPL

0 comments :

Post a Comment