Home » » Miaka minne ndani ya mapango ya Amboni

Miaka minne ndani ya mapango ya Amboni

Written By Bewith Jeddy on Tuesday, November 24, 2015 | 11:30 AM
“Huyo msichana bado mko naye?”
“Tunakuja naye.”
“Hebu mpe simu tumsikie.”
Faiza akapewa simu.
“Hallo!” Akasema akiwa ameiweka simu kwenye sikio.
“Unaitwa nani?”
“Naitwa Faiza”
“Ni kweli kwamba ulikuwa unaishi humu ndani ya pango?”
“Ni kweli.”
“Umeishi kwa muda gani?”
“Miaka minne.”

SASA ENDELEA..
“Miaka minne? Ulikuwa unaishije?”
“Niliishi hivyo hivyo.”
“Hebu tueleze uliingiaje ndani ya hili pango?”
“Sikuingia mwenyewe. Nilishtukia tu nimo ndani ya pango hili.”
“Tuliambiwa kwamba eti uliingizwa na jini, ni kweli?”
“Ni kweli.”
“Huyo jini ndiye unayeishi naye humu?”
“Ndiyo.”
“Tumeambiwa pia kuwa anaua watu wanaoingia katika pango hili, ni kweli?”
“Ndiyo, ni kweli.”
“Ni simulizi ya ajabu sana, sasa sisi tunakuja huko tunafuata huu waya. Ninaamini kuwa tutakutana na utatolewa ndani ya hili pango. Natumaini baada ya kuokolewa utaweza kutueleza vizuri.”
“Sawa kaka. Nashukuru sana.”
Simu ikakatwa upande wa pili. Faiza akampa simu mtu aliyekuwa nayo awali.
“Sasa utaweza kutembea kidogo kidogo?” Mtu huyo akamuuliza Faiza.
“Nitajaribu.”
“Haya twendeni, kwa vile hawa jamaa nao wanakuja tutakutana njiani muda si mrefu.”
Tukaanza tena mwendo. Tulitembea mwendo mrefu bila kukutana na wenzetu hao. Ghafla tuliona mwanga uliomweka kama umeme kisha tukamuona Kaikush ameibuka mbele yetu. Uso wake ulikuwa umegadhibika kama simba.
Alimdaka yule mwenzetu aliyekuwa na bunduki. Tulipoona hivyo nilimshika mkono Faiza tukatoka mbio kwenda mbele.Tulifuata ule waya ulikopitia.
Njia ilikata kona mbele yetu. Tulipokata kona hiyo tukakutana na watu wanakuja. Nikahisi ndiyo wale waliokuwa wanatufuata. Nikashukuru.
“Nyie ni kina nani?” sauti ya mmoja wao ikatuuliza.
Tukajieleza. Tulipowaeleza yaliyomkuta yule mwenzao aliyedakwa na Kaikush wakataka turudi ili wamuokoe.
Nilipoona sasa tulikuwa wengi na miongoni mwetu walikuwemo polisi wawili waliokuwa na bunduki nikakubali tukarudi tena pale mahali.
Tulipofika tuliukuta mwili wa yule mtu ukiwa umelazwa chini. Utosi ulikuwa umetobolewa na chembechembe za ubongo zilikuwa nje.
“Ameshauawa,” nikawaambia.
Jamaa hao walimkagua mwenzao na kuhakikisha kweli ameuawa. Hapo nikawaona wazi walikuwa wamegwaya.
“Sasa huyo jini mwenyewe yuko wapi?” Polisi mmoja akauliza.
“Ameshatoweka,” nikamjibu.
“Sasa tufanyeje?” Mtu mmoja miongoni mwao akauliza.
“Mimi naona turudi tutoke nje ya hili pango halafu wanaohusika watarudi tena wakiwa wamejipanga wachukue miili ya watu waliouawa,” nikawaambia.
Hilo wazo langu lilikubaliwa. Tukaiacha ile maiti na kurudi. Wale watu tayari walikuwa wameshapata hofu.
Tukaanza kurudi huku nikiwaeleza jinsi nilivyoona watu wengine wakiuawa tangu tulipokwama ndani ya pango hilo.
Simulizi zangu zilizidi kuwatia hofu. Kila tulipokuwa tukitembea walikuwa wakitazama nyuma.
“Unaishi naye vipi kiumbe huyo wa ajabu?” Polisi mmoja akamuuliza Faiza.
“Naishi naye hivyo hivyo. Nilikuwa sina la kufanya.”
“Sasa alikupataje mpaka akakuingiza humu?”
“Kifupi ni kuwa alinipata kwetu Bagamoyo. Alinikumba siku ya harusi yangu ndiyo akanileta huku.”
“Alikuletaje?”
“Sijui. Aliponikumba nilipotewa na fahamu. Nilipokuja kuzinduka nikajikuta nipo ndani ya hili pango. Nimekaa humu ndani kwa miaka minne.”
“Unakula nini?” Mtu mmoja akamuuliza.
“Ananiletea vyakula. Kila ninachotaka ananiletea.”
“Kwa nini ulikuwa hutoroki?”
“Nilishajaribu kutoroka mara mbili lakini alinigundua akanikamata na kunipiga sana. Ile mara ya pili alinipiga mpaka nikazirai. Aliniambia kama nitatoroka tena ataniua.”
“Kwa hiyo alitaka uishi humu hadi lini?”
“Aliniambia nitaishi humu hadi kufa kwangu.”
“Sasa ni kwa nini afanye hivyo?” Mtu mwingine aliuliza kwa mshangao.
Faiza akabetua mabega yake.
“Sababu yake siijui. Anachosema yeye ni kuwa mimi amenitunuku.”
Wakati tunaendelea kuzungumza na Faiza tukauona tena ule mwanga ambao ulimweka mbele yetu.
Nilishtuka sana.

0 comments :

Post a Comment