Home » » Mbunge viti maalum afumaniwa

Mbunge viti maalum afumaniwa

Written By Bewith Jeddy on Wednesday, November 25, 2015 | 12:00 PMIMESHANGAZA! Mbunge wa Viti Maalum kupitia chama kimoja cha siasa chenye nguvu nchini ambaye jina lake linahifadhiwa kwa sasa, yupo katika figisufigisu ya ndoa yake kuvunjika kufuatia kufumaniwa na mumewe, Risasi Mchanganyiko linatembea na wewe katika sakata hilo.
Tukio hilo la aibu lilijiri Alhamisi iliyopita kwenye hoteli moja mjini Dodoma ambapo mbunge huyo na mumewe walipiga kambi kwa ajili ya zoezi la wabunge kuapishwa.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, mbunge huyo aliwasili mjini Dodoma na mumewe huyo ambaye ni mfanyabiashara, kwa lengo la kumpa kampani wakati akiapa kiapo cha utii kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
SIKIA SIMULIZI YAKE
“Ilikuwa Alhamisi iliyopita (Novemba 19, 2015), mheshimiwa huyo ambaye amepigana kusaka ubunge kwa miaka mingi bila mafanikio, alikwenda Dodoma na mume wake. Unajua tena, mama anaapishwa lazima baba uwepo.
“Kweli, mama aliapishwa vizuri, akawa mheshimiwa kamili. Shughuli hiyo ilipomalizika, walirudi kwenye ile hoteli waliyofikia,” kilisema chanzo hicho.
RATIBA YA MUME ILICHANGIA
“Sasa kumbe ratiba ilionesha kuwa, baada ya kuapishwa mama na kurudi hotelini, mista asingelala Dodoma. Ilikuwa lazima arudi kwenye makazi yake, mjini Morogoro.
“Waliagana, jamaa akaondoka. Kufika mapokezi aliamua kulipa chumba hicho. Mhudumu akamwambia sawa umelipa chumba chenu, mbona chumba cha dereva bado?
“Jamaa akashtuka! Akamuuliza mtu wa mapokezi, dereva gani? Akajibiwa mkewe alichukua vyumba viwili, cha kwako na cha mtu aliyesema ni dereva wake.”
MUME ATAKA JINA
“Mhudumu bila kufumbafumba macho, akamwonesha kitabu cha mapokezi mume, akaona jina la huyo dereva. Akamwomba mtu wa mapokezi akamwoneshe hicho chumba chenye dereva, akapelekwa.
“Kufika, si akamkuta mwanaume ambaye amekuwa akimtilia shaka siku nyingi kwamba ana uhusiano usiofaa na mke wake.”
PACHIMBIKA
Chanzo kiliendelea kudai kwamba, mwanaume huyo alimpiga sana jamaa mpaka kumchania nguo. Ililazimika ipigwe simu Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma, askari wakaja, wakawachukua wote. Mume, mkewe na mgoni mpaka polisi ambapo walifikia kwenye kitengo cha dawati la jinsia ambako walisuluhishwa hasa ikizingatiwa kwamba, mke huyo ni mheshimiwa mgeni.
MGONI ANUNULIWA NGUO
Habari zaidi zinasema kuwa, ilibidi mgoni anunuliwe nguo nyingine baada ya zile alizovaa wakati wa kichapo kuchanika kutokana na songombingo.
RISASI MCHANGANYIKO NA RPC
Baada ya kuzinyaka taarifa hizo kutoka kwa chanzo, Jumapili iliyopita, gazeti hili lilimpigia simu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, SACP David Misiime na kumuuliza kuhusu kuwepo kwa madai hayo ambapo alijibu:
“Aaah! Mimi sijapata taarifa yoyote. Kwa hiyo sijui kama ni kweli au si kweli, mezani kwangu haijafika!”
MHESHIMIWA ASAKWA
Baada ya kuzungumza na Kamanda Misiime, Risasi Mchanganyiko lilimsaka mheshimiwa huyo kwa simu yake ya kiganjani ambapo mazungumzo yalikuwa hivi:
Mheshimiwa: (anapokea simu) haloo.
Risasi Mchanganyiko: Mzima?
Mheshimiwa: “Mi mzima.”
Risasi Mchanganyiko: (linajitambulisha kwa jina na chombo cha habari).
Mheshimiwa: “Oke, sawa.”
Risasi Mchanganyiko: “Wewe ni mheshimiwa…(anatajwa jina).
Mheshimiwa: “Hapana. Si mimi.”
Risasi Mchanganyiko: “Hapana si wewe au hapana uliyepokea simu si mheshimiwa, bali ni mtu mwingine lakini kwenye namba ya mheshimiwa?”
Mheshimiwa: “Umekosea namba, mimi si ….na wala si namba yake hii.”
Baada ya kukata simu, Risasi Mchanganyiko likampigia simu mume wa mheshimiwa huyo ambapo hali ikawa kama ya kwa mkewe:
“Haloo…”
Risasi Mchanganyiko: “Halo, naongea na…?”
Mume: “Hapana siyo mimi.”
UCHUNGUZI WA RISASI MCHANGANYIKO
Baada ya kugonga mwamba, Risasi Mchanganyiko lilichukua namba za mheshimiwa huyo kutoka kwenye uhifadhi wa kawaida (kitabu cha majina au contact) na kuhamishia kwenye Mtandao wa Instagram ambapo namba hiyo ilitoka na picha ya profile ya mheshimiwa akiwa ndani ya bunge anakula kiapo siku ya Alhamisi.
Bado kama haitoshi, Risasi Mchanganyiko liliingiza namba hiyo kwenye mchakato wa kutuma pesa kwa njia ya mtandao wa simu, likasoma jina la mwanzo la mheshimiwa huyo lakini jina la pili ambalo ni la ukoo si la kwake.
Ilibidi Risasi Mchanganyiko limrudie mnyetishaji wetu na kumwambia kuhusu jina la mheshimiwa kusoma na jina la ukoo ambalo silo.
“Sasa sikia…hilo jina la mbele ni la ukoo wa huyo mume wake. Na watu wake wa karibu wote wanamuita kwa jina hilo la ukoo wa mumewe,” kilisema chanzo chetu.
Katika mtandao wa simu ya mwanaume, jina la pili lilisomeka kama lile la ukoo lililoko mbele ya jina la mkewe.

0 comments :

Post a Comment