Home » » Ukatili wa mume

Ukatili wa mume

Written By Bewith Jeddy on Tuesday, August 11, 2015 | 2:30 AM

 Neema Mwita akiugulia


UKATILI wa mume! Mama mmoja, Neema Mwita aliyeripotiwa na gazeti hili kuwa aliunguzwa na uji wa moto na mumewe Juma Mwita, amefanyiwa upasuaji katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Mama huyo baada ya kumwagiwa uji  na kulazwa takriban mwaka mzima kwenye Hospitali ya Mkoa wa Mara na kushindikana kupona, hivi karibuni aliletwa Muhimbili na Mtangazaji wa Kipindi cha Wanawake Live,  Joyce Kiria ambapo amelazwa kwenye Wodi Namba 24, Jengo la
Sewa Haji.

Akizungumza kwa tabu mama huyo alisema kuwa licha ya kupata kilema cha maisha, anamshukuru Joyce na gazeti hili na wote waliojitokeza kumsaidia kwani hatua aliyofikia sasa inaridhisha na atapona kwani amefanyiwa upasuaji baada ya kuondolewa nyama kwenye paja.

 “Kama unavyoona hata shingo yangu imerekebishwa, nilikuwa nainama tu sikuweza kugeuka kwa sababu iliungana na ngozi ya kifua kutokana na kidonda cha moto, namshukuru Joyce kwa kuja kunichukua Musoma,” alisema Neema.

Neema alipatwa na janga hilo baada ya kuchuma mahindi shambani kitendo kilichomchukiza mumewe aliyeamua kumuunguza kwa uji uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya kusongea ugali.

Naye Joyce alisema: “ Niliguswa sana na unyama aliofanyiwa mama huyu nikaamua kumleta hapa Muhimbili, pia ukatili huu umenisukuma kuandaa pati ya wanandoa itakayofanyika mwezi huu lengo litakuwa kuwakumbusha wanandoa maana ya ndoa na kuwapa ujasiri wanawake wa kufanya kazi ili waweze kusaidiana na waume zao katika maendeleo ambapo kauli mbiu itakuwa ni Mwanamke Piga Kazi.”Hata hivyo, Neema anaomba msaada kwa wasamaria ili aweze kujikimu akiwa hospitali kwani ndugu zake hawana uwezo.
“Naomba msaada kwani ndugu zangu hawana uwezo, licha ya kwamba Napata chakula cha hospitali kuna huduma nyingine zinahitaji fedha,” alisema mama huyo.
Kwa yeyote anayependa kumsaidia mama huyo awasiliane naye kwa namba ya simu 0656151072 au 0756768305, kutoa ni moyo.

0 comments :

Post a Comment