Home » » Mwenye mke achomwa kisu na mgoni!

Mwenye mke achomwa kisu na mgoni!

Written By Bewith Jeddy on Tuesday, June 23, 2015 | 8:37 PM

 Riego Solo (28), mkazi wa Mbezi ya Tangi Bovu, Dar es Salaam anadaiwa kuchomwa kisu kwenye koromeo katika jaribio la kuchinjwa na mgoni wake aliyejulikana kwa jina moja la Jacob akiwa katika harakati za kumzengea mkewe.
  Tukio hilo la kinyume na kawaida ya wanaofumania kufanya uhalifu, lilijiri mwishoni mwa wiki iliyopita, Mbezi ya Tangi Bovu.
Taarifa zilizopatikana katika eneo la tukio zinadai kwamba, Solo alivamiwa na mgoni wake huyo
hatua chache toka nyumbani kwake ambapo wananchi walimsaidia baada ya kupiga kelele na walipofika eneo la tukio walimkuta akitokwa na damu  huku akihangaika chini.
  Akiuguzwa na mke wake aliyemsababishia kujeruhiwa na mgoni wake.

Uwazi baada ya kupata taarifa hizo, lilimfuata Solo nyumbani kwake akiwa ametoka Hospitali ya Mwananyamala, Dar alikolazwa.
Mwanaume huyo alikiri kufanyiwa jaribio la uchinjwaji shingoni na mgoni wake huyo. Alisema:
“Siku hiyo nilikuwa nimetoka kazini. Nilipofika nyumbani, sikukuta chakula, mke wangu alikuwa hajapika. Nikaamua kwenda kununua chakula mahali lakini karibu na hapa kwangu.


Akiwa amepumzika huku akiwa anasikilizia maumivu.

“Nikiwa njiani saa mbili usiku, nilivamiwa na mtu. Alinipiga kwanza kabla ya kuniwekea kisu shingoni, akanijeruhi. Lakini nilimwangalia vizuri nilimjua kuwa ni mgoni wangu, Jacob.
“Tulipambana naye, nikamzidi nguvu lakini tayari alishanijeruhi kwa kunichinja shingoni. Alikimbia huku akiniacha nikigaragara chini. Nilipiga kelele kuomba msaada. Naamini alikuwa na lengo la kuniua ili amrithi mke wangu lakini Mungu ni mkubwa bado nipo hai.
“Huyu Jacob, kuna wakati niliwahi kumuonya kuhusu mke wangu aachane naye, aliniambia amemuacha, hatarudia tena kutembea naye. Lakini cha kushangaza bado akawa anamnyemelea na amekuwa akijificha karibu na hapa kwangu. Watu ndiyo huwa wananiambia, sasa amenijeruhi.
“Kwa kweli Mungu mkubwa, aliyeniokoa wa kwanza ni dada mmoja anayenifahamu, alinikuta nikigaragara chini naye akapiga kelele. Watu walikuja na kunichukua hadi Kituo cha Polisi Kawe na kuchukua PF3 kwa ajili ya matibabu, nikapelekwa Hospitali ya Mwananyamala.
“Nilishonwa nyuzi kadhaa na kuwekewa ‘dripu’,  baadaye niliruhusiwa kurudi nyumbani lakini hali yangu ilibadilika ikabidi nirudishwe tena Hospitali ya TMS. Kwa sasa mke wangu aliyetaka kusababisha nipoteze uhai ndiye huyu anayeniuguza, bado nampenda, sitamwachia.”

0 comments :

Post a Comment