Home » » Ndugu SITA wa Waziri Mwandosya akiwemo dada yake wateketea kwa moto

Ndugu SITA wa Waziri Mwandosya akiwemo dada yake wateketea kwa moto

Written By Bewith Jeddy on Monday, February 9, 2015 | 12:00 PMWaziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya (kushoto) akipewa maelezo na mmoja wa ndugu wa marehemu, George Mwambona kuhusu nyumba (kulia) ilivyoteketea.
Moto ambao chanzo chake hakijafahamika, umewateketeza ndugu sita wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi Maalum, Profesa Mark Mwandosya.
Tukio hilo la aina yake, limetokea usiku wa kuamkia jana eneo la Kipunguni A, jijini Dar es Salaam katika nyumba yenye vyumba vinne waliyokuwa wakiishi familia hiyo.
Waliofariki katika tukio hilo, dada wa Profesa Mwandosya, Celine Egela (50), mume wake Kapteni mstaafu wa Jeshi, David Mpira (60) na mdogo wake Samuel Egela (30).
Wengine ni mtoto wa dada yake waziri, Lucas Mpira (20) pamoja na wajukuu wawili, Celine
Emmanuel (9) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili na Pauline Emmanuel (5).
Mbali ya vifo hivyo, moto huo umeteketeza nyumba yote pamoja na mali zilizokuwamo.
Kwa mujibu wa majirani walioshuhudia tukio hilo, walisema moto huo uliibuka wakati familia hiyo ikiwa imelala.
Josephat Mwakasita, alisema alikuwa mtu wa kwanza kufika eneo hilo la tukio baada ya kusikia sauti ya vilio vya watoto wakiomba msaada kutoka ndani ya nyumba hiyo.
Alisema alipofika eneo hilo alikuta moto ukiwa tayari umetanda sebuleni mwa nyumba hiyo.
“Nilishindwa kuingia kuwaokoa majirani zangu, niliomba msaada kwa majirani wengine ambao walifika hapo tukaanza jitihada ya kuwanasua ndani,” alisema Mwakasita.
Alisema nyuma ya nyumba hiyo kwenye chumba cha Mpira ambaye kwa sasa ni marehemu, walimkuta amesimama dirishani akisali.
“Alikuwa akisema Yesu wangu, Yesu wangu, lakini sikuweza kumuokoa kwa sababu moto ulikuwa tayari umetanda eneo kubwa la nyumba,” aliongeza kusema.
Jirani huyo alibainisha kuwa zoezi la kuudhibiti moto huo lilichukua zaidi ya saa mbili.
MMOJA ANUSURIKA
Yusuph Lima alisema katika tukio hilo, Emmanuel Mpira ambaye ni baba wa watoto wawili waliofariki, alinusurika kutokana na wakati wa tukio alikuwa amelala nje ya nyumba hiyo.

“Emmanuel ambaye kwa sasa yupo hospitali ya Taifa ya Muhimbili akiendelea na matibabu ya maradhi yake pamoja na mshtuko wa tukio hili, alinusurika kwa sababu usiku huo alikuwa amelala nje akilalamika ndani kuna joto,” alisema.
Alisema Emmanuel alishindwa kupiga kelele kutokana na ugonjwa unaomsumbua na baada ya majirani kufika eneo la tukio usiku huo, walimkuta amelala hapo nje. Alisema baada ya tukio hilo, hali yake ilibadilika na kukimbizwa Muhimbili.
MAITI ZALALA PAMOJA
Katika hali isiyo ya kawaida, Mwakasita alisema  mara baada ya tukio, walikuta maiti za watu hao zikiwa zimelala pamoja kwenye vyumba vitatu tofauti.
“Chumba cha kwanza tulikuta maiti ya marehemu Celina na mume wake Mpira, chumba cha pili tulikuta miili ya Samuel na watoto  Celine na Paulina na chumba cha tatu ulikuwapo mwili wa Lucas,” alisema na kuongeza:
“Maiti zote tulizikuta zikiwa zimelala pamoja nadhani walizidiwa na moshi mzito uliotanda kabla ya moto kuwafikia,” aliongeza kusema mkazi mwingine ambaye jina lake hakulitaja.
 VILIO NA SIMANZI VYATAWALA
Waziri Mwandosya ni miongoni mwa viongozi waliofika eneo hilo kushuhudia tukio hilo ambaye alishinda kukamilisha zoezi la ukaguzi wa kile kilichotokea na kulazimika kupelekwa sehemu maalum kukaa.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, alifika eneo hilo kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki.
ZIMA MOTO LAWAMANI
Wananchi wa eneo hilo wamelalamikia kikosi cha zimamoto kwa kitendo chake cha kuchelewa licha ya kupewa taarifa mapema.
“Tulitoa taarifa saa 10:15 usiku lakini zima moto liliwasili hapa saa 1:30 asubuhi wakati tumeshadhibiti moto kwa kiwango kikubwa, huu ni uzembe unaofanywa mara kwa mara na kikosi hiki,” walisema wananchi hao.
Mwananchi mwingine ambaye hakutaja jina lake liandikwe mtandaoni alisema kuwa, baada ya zima moto kuchelewa, walijaribu kupiga namba ya dharura ya polisi lakini  wakati wote ilikuwa ikiita bila kupokelewa.
“Yaani simu ilikuwa inaimba wimbo wa Taifa na hakuna mtu aliyeipokea,” alisema

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Mary Nzuki, alisema uchunguzi  wa tukio hilo unaendelea ili kubaini chanzo cha moto huo.

0 comments :

Post a Comment