Home » » Polisi, TRA wanasa sigara za magendo

Polisi, TRA wanasa sigara za magendo

Written By Bewith Jeddy on Friday, January 30, 2015 | 11:24 AMAskari Kanzu kutoka Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam (nyuma), wakiwa wamewaweka chini ya ulinzi wafanyabiashara wa Mbagala Kuu jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za uuzaji wa sigara za magendo.
KATIKA kukabiliana na uuzaji wa sigara za magendo zisizolipiwa ushuru, Jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa watatu katika maeneo ya Mbagala kwa kuhifadhi na kuuza bidhaa hiyo yenye thamani ya mabilioni ya fedha na kukwepa kodi.
Watuhumiwa hao ni pamoja na Efeso Tweve, Omary Metson na Frank Mrema ambao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote na endapo watakutwa na hatia, huenda wakakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 15 jela au faini ya Sh milioni 50 kwa kosa la kuuza bidhaa iliyotengenezwa kwa kuuzwa nje na hivyo kukwepa kulipa kodi.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Polisi, Simon Sirro ambaye ni Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, msako huo unaendeshwa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Biashara ya magendo katika sigara ilishamiri kuanzia mwaka 2012 kutokana na kile kilichodaiwa kuwa serikali kutoza kodi kubwa kwa bidhaa ya sigara.
Inakadiriwa kuwa asilimia nne ya sigara zote zinazouzwa Tanzania ni za magendo na zina
thamani ya hadi Sh bilioni 30 na takwimu hiyo imepanda kutoka asilimia mbili mwaka 2012.
Sigara hizo zinatengenezwa Tanzania kihalali kwa ajili ya kuuzwa nchi za nje, lakini baadhi ya wafanyabiashara walioko kwenye mtandao wa bidhaa za magendo huzirudisha nchini bila kulipia kodi.
Inadaiwa pia kuwa serikali inapoteza hadi Sh bilioni 10 za kodi kila mwaka kutokana na biashara hiyo ya magendo na kwamba kwa sasa hivi kodi za Tanzania kwa sigara inafikia asilimia 36 ya bei za reja reja za bidhaa hiyo.
Mwaka jana tu Jeshi la Polisi na TRA walikamata sigara milioni 200 katika msako uliofanyika nchi nzima na hilo limedhihirisha kuwa kuna mtandao mkubwa unaojihusisha na biashara hiyo ya magendo.
Bado haijajulikana namna mtandao huo unavyofanya kazi, lakini inaonekana mzigo mkubwa unaingizwa kupitia Reli ya Tazara na pia kwa mabasi yanayoingia Tanzania kupitia mpaka wa Tunduma.
Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC), Paul Makanza, alisema ikiwa serikali itaendelea kuongeza kodi ya sigara kila mwaka huenda ukusanyaji wa mapato ukaendelea kudorora kama inavyofanyika Kenya (asilimia 90) na Uganda (asilimia 86) kwa muda mfupi kwani watu wengi watanunua sigara za magendo.
“Kwa mfano ukusanyaji wa mapato ukipungua kutoka asilimia 96 ya sasa hadi asilimia 90, serikali itapoteza kodi yenye thamani ya Sh bilioni 16. Makanza alisema kwa sasa wastani wa kipato cha Mtanzania kwa siku ni Sh 2,500 ambayo ndio bei ya pakiti moja ya sigara, hivyo wavutaji wengi hawawezi kununua bidhaa hiyo. “Badala yake wanaamua kununua sigara za bei nafuu na wakishazoea inakuwa vigumu kuwashawishi warudi kununua bidhaa halali zilizotozwa kodi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Kampuni na Usalama wa Kampuni ya Sigara Tanzania, Frank Usiri, alipongeza Jeshi la Polisi na TRA kwa kuendesha msako huo na kuviomba vyombo husika kuchukua hatua kali kwa watuhumiwa wa biashara hiyo ya magendo.

0 comments :

Post a Comment