Home » » Lundenga; usitafute mchawi, badilika!

Lundenga; usitafute mchawi, badilika!

Written By Bewith Jeddy on Wednesday, January 7, 2015 | 10:31 AMKWAKO Mkurugenzi wa Lino International Agency, Hashim Lundenga. Bila shaka u-mzima wa afya na unaendelea na michakato yako ya kukufanya mkono uende kinywani.

Binafsi mimi ni mzima wa afya, naendelea na majukumu yangu ya kila siku. Miongoni mwa majukumu yangu ni hili la kukuandikia barua, huwa nawaandikia watu tofauti lakini leo nimekukumbuka wewe kama muandaaji wa shindano kubwa la urembo nchini, Miss Tanzania.
Dhamana uliyokuwa nayo kwa miaka zaidi ya10 sasa kuandaa shindano hilo si ya kubeza. Ni kazi nzito na yenye maslahi makubwa kwa taifa. Warembo ambao wanapatikana kupitia shindano
hilo ndiyo wanaotakiwa kutuwakilisha kwenye mashindano ya dunia.
Ukivurunda huku chini, matokeo yake ni kwenda kuharibu kule juu. Msingi ukiwa mbovu katika mashindano ya wilaya, mkoa na hata mshindi wa Miss Tanzania atakuwa hastahili kutubeba katika mashindano ya dunia.
Nimekuwa nikifuatilia mashindano haya kwa muda mrefu kidogo, natambua ugumu wa mchakato mzima wa kuyaandaa lakini kila mwaka malalamiko ambayo si ya msingi yameendelea kuonekana.
Suala la kwamba matokeo yalipangwa, huo ni wimbo ambao umekuwa ukiimbwa mara kwa mara. Majaji kupendelea, ujanjaujanja unaofanywa na washiriki mara sijui amezaa, ametoa rushwa ya ngono ni mambo ambayo tumechoka kuyasikia.
Ujanjaujanja una mwisho wake na ndiyo maana juzi ukaona kilichotokea kwa mshindi, Sitti Mtemvu ambaye ilibainika amefoji suala la umri. Kabla ya hapo, watu walilalamika kwamba hakustaili tangu siku aliyotangazwa.
Wapo waliomkosoa kwa kushindwa kujieleza au kuzidisha mbwembwe kwa kuongea lugha ya Kifaransa kinyume na masharti ya kujieleza yalivyomtaka. Suala la umri liliibua mjadala mkubwa, likasababisha watu wahoji uhalali wake kiasi cha kumshinikiza mshindi huyo ajivue mwenyewe taji.
Anko nakuheshimu sana, katika kipindi hiki ambacho serikali imekufungia shindano hilo kwa miaka miwili, hauna haja ya kushindana kwa kesi, chukulia kama changamoto. Tengeneza mfumo mzuri ambao utakuwa hauna longolongo pindi utakaporudi kwa mara nyingine.
Hatutegemei kuona mshiriki anaingia katika shindano akiwa hana sifa. Jiridhishe mapema ili kuepuka aibu nzito unayokuja kuipata mwishoni. Epuka vishawishi vya kuchafuka katika hali yoyote.

Hadi kufikia hatua ya kukufungia, najua serikali imevumilia mengi na kuona hakuna haja ya kuendelea kukuvumilia. Hapa lazima uamue kweli kubadilika kama kweli una nia njema katika mashindano haya.
Kila mmoja anapenda kuona Tanzania inafanya vizuri katika tasnia ya urembo. Usiwaangushe, wekeza fedha za kutosha na kama haiwezekani basi tafuta wadhamini wa kutosha watakaoweza kudhamini na kusiwe na longolongo.Kwa leo ngoja niishie hapa, nikutakie maandalizi mema.

0 comments :

Post a Comment