Home » » Mwanamke adaiwa kuteka watoto

Mwanamke adaiwa kuteka watoto

Written By Bewith Jeddy on Tuesday, December 30, 2014 | 9:08 AMMama anayefahamika kwa jina la Sara Zoya akiwa na watoto wake, Imani (14) na Leila (5).

Mama mmoja, Sara Zoya mkazi wa Mabibo Makuburi, jijini Dar es Salaam amekimbilia polisi na kudai kuwa watoto wake walitekwa na ndugu yake  kisha kupelekwa kusikojulikana baada ya kufukuzwa kwenye nyumba yao ya familia.
Sara alidai kuwa ndugu yao huyo aliyefanya kitendo hicho cha utekaji ni Hilda Zoya ambaye anadai aliwateka watoto Imani (14) na Leila (5).
Akizungumza na gazeti hili Sara alisema, alikuwa akiishi na mumewe na baada ya kuachika kwa
mume wake aliamua kurudi kwao kwenye nyumba ya familia na watoto hao wawili. Aliendelea kufafanua:
“Sisi tulizaliwa watoto sita kwa baba na mama mmoja na mimi ndiye mtoto wa kwanza na wazazi wetu wote walishafariki dunia. Mimi nilipoachika niliwataarifu ndugu zangu kuwa nataka kurudi  nyumbani kwetu Mabibo lakini baadhi yao wakanishauri niende nikakae Tabata Kisukuru kwenye nyumba ya mdogo wangu anayeishi Ulaya.
“Mimi sikupenda, nikakataa nikaenda kuishi kwetu, ilipofika Desemba 17 mwaka huu, ndugu yangu Rachel kutoka Ulaya aliyekuja likizo aliniomba nimsindikize kwa mjomba anayeishi Mbezi Beach huku nyuma mdogo wangu Hilda alihamisha vyombo  vyote na kuwachukuwa watoto na kuwapeleka kusikojulikana.
“Niliporudi nyumbani nilikuta milango imefungwa na vitasa vimebadilishwa na kuwekwa mlinzi pia  watoto wangu wawili sikuwakuta.
“Nikaenda kwa mjumbe, mwenyekiti wa  serikali za mitaa kuwaarifu na baada ya hapo nikaenda kutoa taarifa kwenye Kituo cha Polisi cha Mwongozo kilichopo External, wakaniambia nisubiri kwa muda wa saa 24  lakini sikuwaona wanangu na mama yao mdogo Hilda alikuwa hapatikani kwenye simu, ndipo nikaamua kurudi tena  kituoni hapo na kufungua kesi kuhusu kutoonekana kwa watoto, vitu vyangu na mimi kukosa pa kulala.”
Sara amemfungulia kesi mdogo wake Hilda kwa  jalada namba MWP/RB/1655/2014 UTEKAJI WA WATOTO NA WIZI hivyo anasakwa na polisi.Akifafanua zaidi mama huyo alisema: “Siku ya pili watoto walirudi  wenyewe na walipohojiwa walidai walipelekwa Kinondoni kwa Manyanya na mama yao mdogo na kutelekezwa huko na aliwaachia shilingi elfu tano.
“Watoto walisema walipoamka asubuhi waliwauliza wapangaji wa nyumba hiyo wapi walipo na wakaelekezwa kuwa pale ni Kinondoni kwa Manyanya.”
Mtoto Imani alipoulizwa na gazeti hili alikiri kuchukuliwa na mama yao mdogo na kutelekezwa Kinondoni. “Asubuhi tuliwaomba wapangaji watuelekeze namna ya kufika stendi, tukapelekwa tukapanda basi mpaka Makumbusho kisha tukafika nyumbani, tukaelezwa kuwa mama alilala kwa mwenyekiti wa serikali za mitaa.”
Sasa Sara anaomba msaada wa kisheria kwani alidai yeye pamoja na  watoto wake hawana nguo, vyombo na sehemu ya kuishi baada ya kufanyiwa unyama huo na mdogo wake huyo na sasa wamefadhiliwa na  mwenyekiti wa serikali za mtaa wanakoishi.

Source: GPL

0 comments :

Post a Comment