Home » » MMOJA AFARIKI DUNIA, WATANO WAJERUHIWA AJALINI TARIME

MMOJA AFARIKI DUNIA, WATANO WAJERUHIWA AJALINI TARIME

Written By stephen kavishe on Tuesday, July 22, 2014 | 5:00 PM

Dereva wa basi la Zakaria Express, Mbaraka Shamsi (35) mkazi wa Magu akiwa hospitali baada ya ajali.

Roberty Nashoni (48) ambaye ni Mwenyekiti wa Kitongoji cha Sokoni, Sirari-Tarime akitibiwa majeraha katika Hospitali ya Tarime kabla ya kupelekwa Hospitali ya Musoma.
Bi. Bhoke Roberty (28) ambaye ni mke wa Roberty Nashoni wa Sirari, Tarime akipatiwa matibabu kabla ya kupelekwa kutibiwa Hospitali ya Musoma. (Picha na Igenga Mtatiro / GPL, Tarime)
NA IGENGA MTATIRO, TARIME
MTU mmoja, Fatuma Juma Kitumbo (35), amefariki dunia na wengine watano kujeruhiwa katika ajali mbaya ya basi la Zakaria Express lenye namba za usajili T 405 CLT lilipoanguka katika eneo la Sen'gensa Kijiji cha Remagwe, Kata ya Nyamaraga, Wilaya ya Tarime mkoani Mara leo.
Marehemu huyo ambaye ni mtoto wa dada yake mpiga picha wa ITV Musoma, Ahmad Kitumbo, alikuwa akitokea nchini Kenya akielekea jijini Mwanza. Imeelezwa kuwa sababu ya kifo chake ni kutokwa na damu nyingi kutokana na ajali hiyo mbaya.
Ajali hiyo ambayo imethibitishwa na Jeshi la Tarime na Rorya na Kamanda wake Razalo Mambosasa, ilitokea kati ya saa 2.00 hadi 3.00 asubuhi.
Ilidaiwa kuwa chanzo chake ni dereva wa basi hilo kumkwepa binti mmoja aliyekuwa na ngo'mbe wa kukokotwa na jembe na lori lililokuwa barabarani, ndipo basi hilo likaanguka na kusababisha maafa hayo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Halmashauri ya mji wa Tarime, Roberty Onesmo alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na aliwataja majeruhi waliopokelewa hospitalini hapo kwa matibabu kuwa ni dereva wa basi hilo Mbaraka Shamsi (35) aliyeumia kifua, Roberty Nashoni (28) aliyeumia kichwani na mkewe Bhoke Roberty Nashoni (28), aliyeumia kifuani na kichwani, Selfina Abuo (44), Lucy Ngure (22).
Hata hivyo, alisema Bwana Nashoni na mkewe wana hali mbaya na wamepelekwa Hospitali ya Rufaa ya Musoma kuchunguzwa na kwa matibabu zaidi.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilayani hapa, Amos Sagara Nyabikwi aliwatembelea majeruhi wa ajali hiyo katika hospitali hiyo na alifanikisha kuwasafirisha majeruhi hao kupelekwa Hospitali ya Musoma.

0 comments :

Post a Comment