Home » » JAMANI! 'MATESO YANGU ANAYAJUA MUNGU’

JAMANI! 'MATESO YANGU ANAYAJUA MUNGU’

Written By stephen kavishe on Tuesday, July 22, 2014 | 10:04 AM

WAKATI wewe unaishi vizuri na kufanya kila aina ya starehe uitakayo, mambo ni tofauti kwa Ili Chacha (40) ambaye hata mahitaji muhimu kwake ni shida kwa kuwa anasumbuliwa na gonjwa hatari la kansa kwa zaidi ya miaka 14 sasa bila matibabu yoyote.

Ili Chacha (40) anayesumbuliwa na gonjwa hatari la kansa kwa zaidi ya miaka 14.
Chacha ambaye kwa sasa anaishi Ubungo Darajani jijini Dar akitokea mkoani Musoma kwa lengo la kutafuta tiba alikuwa na haya ya kusema:
MAISHA YANGU YAMEJAA HOFU
“Ndugu zangu, sikutegemea kama siku moja ningepatwa na maradhi haya yanayonitesa na kusababisha dunia niione chungu na kuto yafurahia maisha.
“Ugonjwa huu umesababisha nyama za ndani kwa ndani, mashavu na pua yangu kuvimba huku upele mkubwa mfano wa nundu ukinitoka sehemu mbalimbali usoni, yaani jamani mateso yangu anayajua Mungu,” alisema Chacha kwa huzuni.
MIAKA 14 KATIKA UGONJWA
“Kabla ya kupatwa na maradhi haya nilikuwa mwenye furaha kama watu wengine lakini hivi sasa maisha yangu yamebadilika, kweli kama hujafa hujaumbika!
“Ugonjwa huu nilianza kuugua mwaka 2000 nikiwa Musoma, mkoani Mara ambapo kilianza kipele kidogo ambacho sikutegemea kama leo hii kingeyabadilisha maisha yangu kutoka kwenye furaha na kuwa yaliyogubikwa na huzuni.
Chacha akfunguka na kusimulia kwa undani mkasa alionao.
“Wakati nikiwa mwenye afya njema, nilikuwa naishi na kufanya shughuli zangu za ujasiriamali ambazo zilikuwa zikinipa kipato cha kila siku.
“Jambo la kusikitisha ni kwamba, kadiri siku zilivyozidi kwenda mambo yalikuwa tofauti kutokana na kujitokeza uvimbe mkubwa usoni.
“Binafsi sikujua kama uvimbe huo ulikuwa ni kansa nikaudharau na kuamini ungepotea wenyewe.
“Nilipoona unazidi kuwa mkubwa nilipata hofu, nikaamua kuja jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutafuta tiba,” alisema mgonjwa huyo.
AINGIA DAR BILA KUWA NA NDUGU
Chacha kwa shida aliongeza: “Mwaka 2010, nilifika Dar huku nikiwa sina ndugu, nikaanza kuishi kwa kutangatanga kwa kipindi chote hicho na kujaribu kwenda hospitali mbalimbali bila mafanikio,” alisema Chacha.
AGUNDULIKA ANA KANSA
 “Baada ya kuhangaika sana nilikwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambapo nilipimwa na kugundulika uvimbe niliokuwanao ulikuwa kansa.
“Taarifa hiyo ilinisikitisha sana kwani niliwahi kusikia kwamba maradhi hayo yalikuwa hatari.
“Hata hivyo, niliamini kama ningepata tiba ya uhakika ningepona na kuendelea na maisha kama zamani.
“Daktari aliyenipima aliniambia ili kupona maradhi hayo nilipaswa kwenda kufanyiwa upasuaji nchini India na gharama zake ni shilingi milioni kumi.
“Tangu nilipoambiwa hivyo nimepoteza matumaini ya kuendelea kuishi kwa sababu sina uwezo wa kupata kiasi hicho cha fedha na wala sina ndugu anayeweza kunisaidia kuzipata, hivyo nimekuwa mtu wa kuishi kwa mateso usiku na mchana.
Ndugu msomaji, ili kuokoa maisha yake, Chacha anahitaji msaada wa hali na mali kwani licha ya kuteswa na kansa ana uhitaji wa chakula, malazi nk.
Kama umeguswa na matatizo yake unaweza kumsaidia kupitia namba 0652 006 910.

0 comments :

Post a Comment