Home » » FAHAMU UGONJWA WA FIGO

FAHAMU UGONJWA WA FIGO

Written By stephen kavishe on Tuesday, July 22, 2014 | 11:30 AMNa Dk. A. Mandai,   Simu: +255 717 961795 au +255 754 391743
FIGO ni miongoni mwa viungo muhimu katika mfumo wa utendaji kazi wa mwili wa binadamu.
Kwa kawaida  mwili wa binadamu una figo mbili zenye maumbo yanayofanana, yakiwa yamejificha nje ya utando unaozunguka tumbo chini ya mbavu.


Figo hizo zikipata madhara tunasema mtu fulani anaumwa figo na mbaya zaidi ni kwamba hautibiki kirahisi na gharama za matibabu huwa ni kubwa sana.Kazi kuu za figo ni kuchuja vitu mbalimbali pamoja na sumu katika damu, kusaidia kuhifadhi, kudhibiti kiwango cha maji na madini (electrolytes) mwilini.
Figo huchuja vitu hivyo pamoja na maji yaliyo mwilini na kutengeneza mkojo, huchuja pia maji yasiyohitajika mwilini huku yakinyonya madini na kemikali muhimu kuzirudisha katika mzunguko wa damu na kutoa nje uchafu usiohitajika.
Kazi nyingine za figo ni pamoja na kusaidia kutengeneza kiasili cha erythropoletin ambacho ni muhimu katika utengenezaji wa chembechembe nyekundu za damu, hupokea asilimia 25 ya damu na kila figo ina chembechembe hai ndogo milioni moja, pia kusaidia kudhibiti na kurekebisha shinikizo la damu mwilini (blood pressure).
Zipo sababu kadhaa zinazosababisha maradhi katika figo kwa binadamu ikiwamo matumizi mabaya ya dawa hasa za maumivu, baadhi ya dawa za Kichina, uvutaji wa sigara na  unywaji wa pombe kupita kiasi.
Aina za ugonjwa wa figo
Kuna aina mbili kuu za ugonjwa huu, kwanza ni ile ya figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla na muda mfupi; pili ni ile ya figo kushindwa kufanya kazi polepole na kwa muda mrefu.
Figo kushindwa kufanya kazi polepole na kwa muda mrefu huharibiwa taratibu na kuendelea kupunguza uwezo wake wa kufanya kazi kadiri siku zinavyokwenda.

Dalili za aina hii ya ugonjwa huchelewa kujitokeza na wakati  mwingine mwenye tatizo hajisikii dalili yoyote, hadi pale inapotokea akaugua ugonjwa mwingine na daktari kuhisi tatizo, ndipo hugundulika kuwa na ugonjwa huo baada ya vipimo.
Sababu kubwa ya figo kushindwa kufanya kazi ghafla ni kupungua kwa mzunguko wa damu kwenye figo, kemikali za mwilini au kushambuliwa na sumu.
Kushuka kiwango cha mzunguko wa damu humpata mtu anayetapika sana na hanywi maji ya kutosha, anayeharisha sana na hanywi maji ya kutosha na wale ambao hupoteza damu nyingi kama vile kwenye ajali.

Sababu nyingine ni mgonjwa kuwa na ugonjwa wa moyo,  moyo kushindwa kusukuma damu kwa ghafla, au waliougua maradhi ya moyo kwa muda mrefu.
Mtu kuwa na kemikali zinazotokana na kutumia dawa iliyo na mzio kwa mtumiaji, dawa zinazosababisha mkojo utoke kwa wingi, na baadhi ya dawa za malaria.
Tatizo la figo kushindwa kufanya kazi kwa ghafla pia humpata mtu ambaye ana bakteria kwenye mzunguko wa damu, ambao wanaweza kusababisha homa  ‘Septicemia’ na kuugua malaria.
Sababu zinazofanya figo ishindwe kufanya kazi taratibu na kwa muda mrefu na hatimaye kushindwa kabisa kuwa ni presha kuwa juu, kisukari, magonjwa yanayosababishwa na bakteria, HIV, saratani na sumu mbalimbali zinazoingia mwilini.

DALILI
Dalili ya kwanza ni kupungua kwa kiasi cha mkojo, maji kujaa mwilini, madini ya mwili kuwa juu hasa ya ‘potasiamu’, asidi nyingi,  matatizo katika moyo, ubongo, kukosa hamu ya kula na kudhoofika mwili.
Nyingine ni kwa wagonjwa ambao  hawagunduliki mapema ni kuvimba macho wakati wa asubuhi na uvimbe kupungua baadaye,  kupungukiwa damu mwilini kama dalili za kwanza (figo ikishindwa kufanya kazi ya kusaidia kutengeneza damu).

0 comments :

Post a Comment