Home » » BOSI ALIVYONUSURIKA KUUAWA KWA RISASI

BOSI ALIVYONUSURIKA KUUAWA KWA RISASI

Written By stephen kavishe on Thursday, July 17, 2014 | 8:09 AM

INASIKITISHA! Watu wasiojulikana wamemshambulia kwa risasi na mapanga Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Geita, Juma Kimisha na msafara wake na kusababisha kiongozi huyo kukimbizwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Mwanza ili kuokoa uhai wake.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Geita, Juma Kimisha akiwa Hospitali ya Wilaya ya Kahama Kitengo cha Bima.
Akizungumza kwa shida katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama Kitengo cha Bima ambapo alipatiwa huduma za matibabu kwa lengo la kuokoa uhai wake kabla ya kupewa rufaa ya matibabu kwenda Bugando jijini Mwanza, Kimisha alisema mbali ya kujeruhiwa waliibiwa mali zao.
Alisema tukio hilo lilitokea Julai 3, 2014, saa mbili na nusu usiku katika Kata ya Igusule wilayani Nzega wakiwa hatua chache kufika katika mpaka wa Mikoa ya Tabora na Shinyanga, walipokuwa wakitoka jijini Tanga katika maadhimisho ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAAT).
Mwenyekiti huyo alisema akiwa katika gari la Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu lenye namba za Usajili SM 10032 (pichani) lililokuwa likiendeshwa na Joseph Dutu Machibya, walikuta kizuizi cha mawe makubwa barabarani katika eneo walilotekwa na kuwalazimu kusimama ndipo waliposhtukia mvua za risasi zikilisakama gari lao.
Dereva Joseph Dutu Machibya aliyejeruhiwa pia katika tukio hilo.
Kimisha alisema risasi hizo zilizosambaratisha vioo vya gari lao zilidumu kwa takriban dakika 20 ndipo kundi la watu zaidi ya 30 lilipowazingira kwa mbali likiwa na bunduki, mapanga, nondo na marungu huku likiwataka wasalimishe silaha, ambapo waliwaeleza hawakuwa na silaha ya aina yoyote.
Alisema baada ya watu hao kujiridhisha kuwa hawana silaha ndipo lilipowavamia kwa kufungua milango na kuwatoa nje huku wakiwashambulia kwa silaha walizokuwa nazo na kuwashurutisha kuwapatia mali walizokuwa nazo.
Hata hivyo, katika hatua ambayo walishindwa kuamini ni watu hao wanaosadikiwa kuwa majambazi, kitendo cha kuwarudishia runinga yao waliyotumia kwa ajili ya maonyesho katika maadhimisho ya ALAAT, huku yakikwapua simu mbili za kila mmoja na pesa taslimu kiasi cha shilingi milioni moja na nusu.
 Baada ya uhalifu huo waliwaruhusu waendelee na safari yao huku wakiwashurutisha wenzake wambebe na kumuingiza ndani ya gari jambo ambalo hakuelewa sababu yake hadi alipofika Kituo cha Polisi, Kata ya Kagongwa wilayani Kahama.

Gari la Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu lenye namba za Usajili SM 10032 lililoshambuliwa kwa risasi katika mkasa huo.

Katika kituo hicho cha polisi walipofika kutoa ripoti ndipo alipobaini alijeruhiwa kwa risasi katika paja lake la mguu wa kushoto pamoja na mgongoni ambapo pamoja na wenzake walichukua hati namba tatu ya polisi ‘PF 3’ na kukimbizwa Hospitali ya Wilaya ya Kahama.
Kaimu Mganga Mkuu, Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Dkt. Deo Nyaga alisema waliwapokea majeruhi hao saa sita usiku na kuanza kuwapatia matibabu mara moja na ilipofika asubuhi waliwaruhusu kurejea makwao; dreva wa gari hilo Machibya, Afisa Biashara wa Halmashauri ya Ushetu, Selestine Lufundisha na mkulima wa zao la Tumbaku toka Kata ya Ulowa, Pendo Shiengo ambao wote walikuwa katika gari hilo.
Dkt Nyaga alisema walifanikiwa kumtoa risasi ya paja mwenyekiti huyo huku wakilazimika kumpiga X – Ray kubaini madhara ya risasi iliyomuingia mgongoni na kugundua risasi hiyo imejikita katikati ya ubavu na uti wa mgongo inchi moja na nusu kutoka mahali ulipo moyo.
“Tuliketi madaktari tukabaini kesi hii ni kubwa kwetu hivyo tukalazimika kumpa rufaa akatibiwe Bugando jijini Mwanza,” alisema Daktari Nyaga.
Jeshi la Polisi wilayani Kahama limethibitisha kutokea kwa matukio hayo na kubainisha tayari wameishaanza uchunguzi kwa kushirikiana na askari wa Wilaya ya Nzega ili kuhakikisha waharifu hao wanawatia mbaroni na mkondo wa sheria unachukua nafasi dhidi yao.

0 comments :

Post a Comment